KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Maandalizi ya kumwapisha rais Kenyatta yamalizika

Rais Uhuru Kenyatta, akiwa kazini katika siku zilizopita
Rais Uhuru Kenyatta, akiwa kazini katika siku zilizopita State House Kenya

Marais 11 kutoka barani Afrika akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ni miongoni mwa wageni mashuhuri wanaotarajiwa kushuhudia kuapishwa kwa rais Uhuru Kenyatta kuhudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho siku ya Jumanne jijini Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Kasarani kuanzia saa mbili asubuhi.

Wizara ya Mambo ya nje nchini humo, imeliambia Gazeti la kila siku la Daily Nation kuwa mataifa mengine 13 yatatuma wawakilishi wao katika sherehe hizo.

Marais wanaoripotiwa kuthibitisha kushuhudia kuapishwa kwa Kenyatta ni pamoja na rais Yoweri Museveni wa Uganda, rais wa Botswana Ian Khama, Paul Kagame (Rwanda), John Pombe Magufuli (Tanzania).

Wengine ni Edgar Lungu (Zambia), Ismaïl Omar Guelleh (Djibouti), Hage Geingob (Namibia), Faure Gnassingbé (Togo), Mohamed Farmajo wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn.

Kenyatta anatarajiwa kula kiapo na kuanza kuongoza nchi iliyogawanyika kisiasa, huku upinzani ukisema kuwa hautamtambua kama rais wa Kenya.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, anatarajiwa kuwaongoza wafuasi wake katika mkutano wa hadhara jijini Nairobi, kuwakumbuka watu zaidi ya 20 waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi wiki mbili zilizopita, wakati wa maandamano ya kumkaribisha nchini baada ya kurejea kutoka Marekani.