KENYA-SIASA

Ulinzi waimarishwa Nairobi kabla ya Kenyatta kuapishwa

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuapishwa Jumanne hii Novemba 28, 2017.
Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuapishwa Jumanne hii Novemba 28, 2017. REUTERS/Thomas Mukoya

Ulinzi umeimarishwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi pamoja na miji mingine huku rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuapishwa leo Jumanne kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Muungano wa upinzani, NASA, umepanga mkutano wa hadhara jijini Nairobi, kuwakumbuka watu zaidi ya 20 waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi wiki mbili zilizopita, wakati wa maandamano ya kumkaribisha kiongozi wa muungano huo Raila Odinga nchini baada ya kurejea kutoka Marekani.

Bw Odinga alisisitiza kwamba mkutano huo utafanyika katika uwanja wa Jacarada, Nairobi, kilomita kumi kutoka uwanja wa Kasarani ambapo sherehe ya kuapishwa kwa Bw Kenyatta itakuwa inaendelea.

Kuna hatari ya kutokea makabiliano makubwa kati ya wafuasi wa upinzani n apolisi, kwani siku ya Jumatatu polisi isisitiza kwamba hakutakuwa na mkutano mwingine Nairobi ila sherehe ya kumuapisha Bw Kenyatta.

Zaidi ya marais 20 kutoka barani Afrika akiwemo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ni miongoni mwa wageni mashuhuri wanaotarajiwa kushuhudia kuapishwa kwa rais Uhuru Kenyatta.

Marais wanaoripotiwa kuthibitisha kushuhudia kuapishwa kwa Kenyatta ni pamoja na rais Yoweri Museveni wa Uganda, rais wa Botswana Ian Khama, Paul Kagame (Rwanda), John Pombe Magufuli (Tanzania).

Wengine ni Edgar Lungu (Zambia), Ismaïl Omar Guelleh (Djibouti), Hage Geingob (Namibia), Faure Gnassingbé (Togo), Mohamed Farmajo wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn.

Kenyatta anatarajiwa kula kiapo na kuanza kuongoza nchi iliyogawanyika kisiasa, huku upinzani ukisema kuwa hautamtambua kama rais wa Kenya.

Bw Kenyatta alipata asilimia 98 ya kura katika uchaguzi wa marudio, ushindi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu iliyofutilia mbali kesi mbili zilizokuwa zimewasilishwa na wanaharakati wawili na mbunge wa zamani kupinga uchaguzi huo.