KENYA-MAREKANI-SIASA

Marekani yaitaka NASA kuzungumza na rais Kenyatta

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (NASA) Raila Odinga akiandamana na wafuasi wake, Kawangware Nairobi, Kenya Oktoba 29, 2017.
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (NASA) Raila Odinga akiandamana na wafuasi wake, Kawangware Nairobi, Kenya Oktoba 29, 2017. REUTERS/Thomas Mukoya

Balozi wa Marekani nchini Kenya Robert Godec ameutaka muungano wa upinzani NASA kuwa tayari kulegeza masharti ya madai yao na kuwa na mazungumzo na rais Uhuru Kenyatta.

Matangazo ya kibiashara

Bw Godec ametoa kauli hii licha ya viongozi wa muungano huo kusisitiza tarehe 30 Raila Odinga na naibu wake Kalonzo Musyoka wataapishwa.

Katika mazungumzo tofauti na kiongozi wa wachache bungeni John Mbadi na mmoja wa viongozi wa muungano huo Moses Wetang’ula, balozi Godec amekiri kuwa NASA na Jubilee wana mawazo tofauti kuhusu kinachotakiwa kujadiliwa lakini akawataka kuwa wazalendo.

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, Raila Odinga yeye na kinara mwenzake Kalonzo Musyoka wataapishwa mwisho wa mwezi huu, kama rais na naibu raia wa watu.

Wafuasi wao wamekuwa wakisema wanasubiri siku hiyo, huku wafuasi wa rais Uhuru Kenyatta wakihofia kuwa hatua hiyo itayumbisha uchumi lakini pia kuzua mzozo mpya wa kisiasa.

Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA wametangaza kampeni ya kitaifa kuhamasisha wafuasi wao kujitokeza kwenye sherehe za kuapishwa kwa kiongozi wao Raila Odinga na naibu wake Kalonzo Musyoka tarehe 30 ya Mwezi huu.

Vinara hao wawili wamesema sasa tarehe imeshaafikiwa na kwamba hawatashinikizwa na wafuasi wao kuapa na badala yake wataapishwa kwa kufuata maelekezo ya washauri wao.

Akihutubia kwenye mkutano wa baraza la wananchi mjini Kakamega, Raila Odinga alisema kula kwao kiapo hakuna uhusiano na wao kuwa na uchu wa madaraka lakini wanatimiza wajibu.

Tayari rais Uhuru Kenyatta ametangaza kutowavumulia wanasiasa ambao watajaribu kutatiza usalama wa nchi hiyo na kukiuka katiba ya nchi, akisisitiza kuwa tayari kwa mazungumzo yenye tija lakini sio ya kisiasa.