BURUNDI-KURA YA MAONI-SIASA

Kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba kufanyika mwezi Mei nchini Burundi

mmoj wa wapiga kura katika eneo la Buye,  alikozaliwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
mmoj wa wapiga kura katika eneo la Buye, alikozaliwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza. PHOTO / PHIL MOORE

Serikali ya Burundi inaandaa kura ya maoni mwezi May mwaka huu kuhusu marekebisho ya katiba yatakayomruhusu rais Pierre Nkurunziza kusalia madarakani hadi mwaka 2034 na kutoa mamlaka makubwa kwa rais hatua ambayo imelaaniwa na upinzani.

Matangazo ya kibiashara

Kampeni za kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba nchini Burundi na uhamasishaji ilianza mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka uliopita.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ndiye aliongoza kampeni hiyo kuhamasisha raia kuhusu kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba.

Pierre Claver Ndayicariye msimamizi wa tume ya kusimamia uchaguzi alifahamisha kuwa kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba  inatarajiwa kufanyika ifikapo  Mei mwaka 2018.

Wadadisi wanasema hiyo ni mbinu ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutaka kusalia madarakani, baada ya kujaribu kurekebisha mwaka 2014 kipengele cha katiba kinachomzuia kuwania muhula wa tatu bila mafanikio.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mpango huo unahusisha kuidhinishwa kwa rasimu ya katiba ambayo itamuwezesha kuwania urais kwa mihula miwili zaidi ya miaka saba kila muhula.

Kwa mujibu wa maafisa waandamizi wa chama tawala cha CNDD-FDD ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamesema muhula wa tatu na wa mwisho kwa Nkurunziza ni huu anaohudumu hadi mwaka 2020, lakini anataka asalie madarakani hadi mwaka 2034.

Muungano wa wanasiasa wa upinzani walio uhamishoni CNARED wamekosoa mpango wa Nkurunziza wa kurekebisha katiba ya nchi wakiutaja kuwa ni kutaka asalie mamlakani. CNARED wamesema hawatakubaliana na jambo hilo.