KENYA-SIASA

Rais Kenyatta atangaza Baraza la Mawaziri huku Odinga akipanga kuapishwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta .
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta . State House Kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza Baraza lake la Mawaziri, miezi miwili baada ya kuapishwa kutoakana na Uchaguzi mpya wa urais uliofanyika mwezi Oktiba mwaka uliopita na kumpa ushindi baada ya mpinzani wake Mkuu Raila Odinga, kujiondoa kwenye Uchaguzi huo.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa Mawaziri walioteuliwa ni pamoja na Raychelle Omamo ambaye ameteuliwa tena kuwa Walinzi wa Ulinzi huku Waziri wa zamani wa Mambo ya nje Amina Mohammed akiteuliwa kuwa Waziri wa Elimu.

Waziri mpya wa mambo ya nje ni Monica Juma. Kabla ya kuapishwa kwa Mawaziri hao 21, ni sharti bunge lijadili na kuwahoji Mawaziri hao kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Wachambuzi wa siasa wanasema uteuzi huu, unamaliza matumaini ya uwezekano wa Kenyatta na Odinga kuunda serikali ya pamoja, wakati huu nchi hiyo ikiendelea kushuhudia mvutano wa kisiasa.

Muungano wa upinzani NASA, umepanga kumwapisha Odinga wiki ijayo kama rais wa watu jijini Nairobi.

Hadi sasa juhudi za kuwepo kwa mazungumzo kati ya rais Kenyatta na Odinga hazijafua dafu licha ya Marekani kujaribu kushawishi pande zote kuja kwenye meza ya mazungumzo.

Umoja wa Mataifa ulimtuma rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo hivi kwenda kusuluhisha mvutano huo, lakini ripoti zinasema kuwa hakufanikiwa.