KENYA-SIASA

Odinga kuapishwa Jumanne hii, Polisi yapiga marufuku sherehe yoyote Uhuru Park

Kiongozi wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinda, Novemba 28, 2017.
Kiongozi wa muungano wa upinzani, NASA, Raila Odinda, Novemba 28, 2017. REUTERS/Baz Ratner

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, unatarajia kumuapisha kiongozi wake Raila Odinda kuwa rais wa watu nchini Kenya. Hali ya wasiwasi imetanda nchini Kenya kufuatia msimamo huo wa NASA wa kumuapisha Raila Odinga.

Matangazo ya kibiashara

Kituo cha habari cha kibinafsi cha Citizen kimearifu kuwa maafisa wa polisi wameamrishwa kuondoka katika uwanja wa Uhuru Park na wafuasi wa upinzani wameanza kuingia uwanja wa Uhuru Park baada ya polisi kuondoka.

Baadhi wanazunguka uwanja huo wakiimba 'Uhuru Must Go'.

Awali serikali imeonya kuwa hatua ya kuapishwa kwa Bw Odinga ni uhaini wa kiwango cha juu

Jana Jumatatu jio NASA ulisema maandalizi yamekamilika kuelekea kumwapisha kiongozi wake Raila Odinga kama rais watu leo Jumanne katika bustani ya uhuru jijini Nairobi.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa NASA Norman Magaya aliwaambia wafuasi wa NASA kuwasili katika bustani hiyo kufikia saa mbili asubuhi kwa maandalizi ya kumwapisha Odinga na Naibu wake Kalonzo Musyoka saa nne asubuhi.

Licha ya hakikisho hilo, wasiwasi umezuka kuhusu iwapo shughuli hiyo itafanyika katika bustani hiyo baada ya jeshi la Polisi kupiga marufuku mkusanyiko wa watu katika bustani ya Uhuru Park..

Kabla ya Polisi kupiga marufuku hayo, serikali ya Kaunti ya Nairobi ilitangaza kufunga bustani hiyo kwa ukarabati.

Kamanda wa jiji la Nairobi Japhet Koome, alisema hataruhusu yeyote kuonekana katika bustani hiyo.

“Siwezi kuruhusu watu kwenda kuumizana katika bustani ya Uhuru Park,” alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi wa NASA walisema shughuli za kumwapisha Odnga lazima zifanyike baada ya kumtuhumu rais Kenyatta kukataa mazungumzo ya kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita.

Kiongozi wa Kanisa la Anglikana nchini humo Jackson Olesapit ametaka Odinga kuruhusiwa kuendelea na shughuli hiyo kwa amani, ili kuepuka makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa NASA.

Raila Odinga anadai alishinda uchaguzi urais wa tarehe 8 Agosti 2017.

Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya uchaguzi huo wa Agosti na kuagiza uchaguzi urudiwe, lakini Bw Odinga akasusia.

Odinga amesema hatambui ushindi wa Bw Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa marudio wa 26 Oktoba.

Kenyatta amekuwa akisema kuwa, mazungumzo pekee anayotaka ni yale yanayolenga kuleta maendeleo nchini humo.