KENYA-SIASA

Raila Odinga aapishwa kama "rais" licha ya kushindwa uchaguzi

Maelfu ya wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga walikusanyika Nairobi leo Jumanne kumuapisha kiongozi wao kama "rais" licha ya kushindwa katika uchaguzi uchaguzi mwaka uliopita.

Kiongozi wa muungano wa upinzani (NASA) Raila Odinga.
Kiongozi wa muungano wa upinzani (NASA) Raila Odinga. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo serikali ilipiga marufuku vyombo vya habari kurusha hewani sherehe hiyo.

Tukio hili lilitangazwa na upinzani miezi mitatu baada ya kususia uchaguzi, huku Raila Odinga akisema kuwa aliibiwa kura ambzo zilimpa yeye ushindi.

Mapema wiki hii polisi ilitangaza kwamba itazuia sherehe yoyote katika uwanja wa Uhuru Park.

Odinga amechukua hatua hii licha ya onyo la serikali ya rais Uhuru Kenyatta kuwa itamfungulia mashtaka ya uhaini.

“Mimi Raila Amollo Odinga, nikiwa natambua wito, naapa kuwa rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya,” alisema Odinga huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Akiwahotubia wafuasi wake, Odinga amesema wananchi wa taifa hilo wameamua kuondoa utawala wa kidikteta ulioletwa na wizi wa kura.

Aidha, amesema kuwa ametimiza ahadi aliyoitoa kwa Wakenya kuwa ataapishwa kama rais wa wananchi.

Odinga, mwenye umri wa miaka 72, ni mkongwe wa siasa ya Kenya ambaye anasema kuwa udanganyifu wa kura ulikumzuia kushinda uchaguzi wa urais mara kadhaa katika siku za nyuma na anakataa kukubali uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta mwaka jana, baada ya miezi kadhaa ya machafuko ambapo, kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu, watu 92 waliuawa.

Uchaguzi wa kwanza ulifanyika tarehe 8 Agosti 2017, ambapo Uhuru Kenyatta aliibuka mhindi, lakini matokeo yake yafutiliwa mbali kwa uamuzi wa kihistoria wa Mahakama Kuu na uchaguzi mpya ulifanyika mnamo Oktoba 26. Bw Odinga alisusia uchaguzi huo baada ya kudai kuwa uchaguzi huo hautakua huru, Wakati Uhuru Kenyatta alishinda kwa asilimia 98 ya kura. Alitawazwa rasmi mwishoni mwa mwezi Novemba.