TANZANIA-TANZIA

Watanzania waomboleza kifo cha mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Kingunge Ngombale Mwiru siku za uhai wake
Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Kingunge Ngombale Mwiru siku za uhai wake www.thecitizen.co.tz

Rais wa Tanzania John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Kingunge Ngombale-Mwiru.

Matangazo ya kibiashara

Mwanasiasa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 87 amefariki dunia alfajiri ya kumkia leo Jumanne Februari 2 mwaka 2018 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na mbwa akiwa nyumbani kwake Disemba 22 mwaka jana.

Taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya rais Ikulu imemnukuu rais Magufuli akisema Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye aliotoa mchango mkubwa katika harakati za kuwania uhuru Tanzania.

“Mzee Kingunge ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa mzalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na kwa nidhamu,”amesema Rais Magufuli.

Kufuatia msiba huo serikali ya Tanzania imewapa pole wanafamilia na wote walioguswa na msiba wa kiongozi huyo.

Kingunge Ngombale-Mwiru alizaliwa Mei, 30 mwaka 1930 na aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne na mwaka 2015 alijiondoa katika Chama cha Mapinduzi na kujiunga na upinzani.

Ripoti na Mwandishi wa RFI Kiswahili, Fredrick Nwaka.