KENYA-SIASA-DEMOKRASIA

Mwanasiasa mwingine wa upinzani akamatwa nchini Kenya

Kiongozi wa upinzani  aliyejiapisha kama rais wa watu hivi karibuni  Raïla Odinga
Kiongozi wa upinzani aliyejiapisha kama rais wa watu hivi karibuni Raïla Odinga REUTERS/Baz Ratner

Polisi nchini Kenya wamemkamata mwanasiasa mwingine wa upinzani, baada ya kuapishwa kwa kiongozi wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga kuwa rais wa watu wiki hii. Ripoti zinasema  mwanasiasa huyo ameachiwa huru Jumamosi jioni.

Matangazo ya kibiashara

Mbunge wa Makadara George Aladwa anakuwa mwanasiasa wa tatu kukamatwa akiwa nyumbani kwake jijini Nairobi.

Msemaji wa jeshi la Polisi nchini humo Charles Owino amethibitishwa kukamatwa kwa mbunge huyo, na kueleza kuwa pia anachunguzwa kuhusu uvamizi wa mmoja wa viongozi wa NASA Kalonzo Musyoka, ambaye wiki hii alishambuliwa nyumbani kwake.

Wanasiasa wengine waliokamatwa ni Miguna Miguna na TJ Kajwang ambaye ameachiliwa huru kwa dhamana.

Wakati uo huo, licha ya Mahakama kuagiza kufunguliwa kwa mitambo ya Runinga tatu nchini humo siku ya Alhamisi, bado mitambo hiyo haijafunguliwa.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Mashirika ya kiraia, yamelaani hatua ya serikali ya Kenya kuzima mitambo ya Citizen TV, NTV na KTN News kwa madai kuwa vituo hivyo vingeonesha moja kwa moja kuapishwa kwa Odinga.

Mwanaharakati Okoiti Omtata alikwenda Mahakamani wiki hii, na kufanikiwa kupata agizo la kufunguliwa kwa mitambo hiyo lakini, Tume ya Mawasiliano nchini humo, imemzuia mwanaharakati huyo kuwasilisha agizo hio.

Hatua hii imeelezwa kama ukiukwaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya Habari nchini Kenya.