KENYA-SIASA

Mvutano wa kisiasa waendelea Kenya baada ya Odinga kujiapisha

DWakenya wakisilikiza hotuba ya Raila Odinga, Kisumu mnamo Oktoba 31, 2017.
DWakenya wakisilikiza hotuba ya Raila Odinga, Kisumu mnamo Oktoba 31, 2017. REUTERS/Baz Ratner

Maswali yameendelea kuibuka nchini Kenya kuhusu mustakabali wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye wabunge wake wameendelea kukamatwa na vyombo vya usalama kwa mahojiano.

Matangazo ya kibiashara

Wanasiasa wa upinzani wamesema watafungua kesi kupinga kuendelea kukamatwa kwa wenzao wanaodaiwa kuwa walipanga na kushiriki sherehe za kuapishwa kwa kinara wa upinzani Raila Odinga, kiapo ambacho serikali inasema kilikuwa kinyume cha Sheria.

Mpaka sasa wabunge watatu wa upinzani walioshiriki kwenye kuapishwa kwa Odinga wamekamatwa na wanahojiwa na polisi kuhusiana na ushiriki wao huku, maswali mengi ya kibakia ni kwanini serikali haimkamati Raila Odinga ambaye ndiye alikula kiapo kama rais wa wananchi juma lililopita.

Serikali ya chama tawala cha Jubilee imeendelea kuwaandama wanasiasa wa upinzani ambapo imetangaza kuwanyang’anya walinzi, silaha wanazomiliki na sasa watanyang’anywa hati zao za kusafiria.

Juma lililopita pia Serikali ilitangaza kuvifungia vituo vitatu vya televisheni ikivituhumu kwa uchochezi hatua iliyokosolewa na wanaharakati na hata nchi ya Marekani.