KENYA-MAANDAMANO-VYOMBO VYA HABARI

Polisi yasambaratisha maandamano dhidi ya serikali

Polisi ikitawanya waandamanaji, Nairobi, Kenya,
Polisi ikitawanya waandamanaji, Nairobi, Kenya, REUTERS/Thomas Mukoya

Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika miji mbalimbali nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Nairobi.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano makubwa yalitrajiwa hii leo Nairobi kuishinikiza serikali kuvifungua vyombo vitatu vya habari nchini humo vilivyofungiwa kupeperusha matangazo kwa siku ya saba leo.

Maandamano haya yanajiri wakati viongozi wa upinzani waliokamatwa kwa madai ya kushiriki njama ya kumuapisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama rais.

Serikali ilizifunga stesheni tatu za televisheni NTV, Citizen na KTN kwa madai kuwa vilipanga kupeperusha moja kwa moja matangazo licha ya onyo kutofanya hivo.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu, waandishi habari na baadhi ya wananchi walipanga kufanya maadamano hii leo Nairobi kuishinikiza serikali kutii amri ya mahakama.

Waandalizi wa maandamano hayo wanaishtumu serikali wakidai imekiuka haki za kibinadamu, kuendeleza mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari kando na kupunguza uhuru wa demokrasia nchini kwa kutoheshimu katiba.

Hivi karibuni Mahakama iliagiza serikali kufungua vituo vitatu habari vilivyofungwa na serikali.