KENYA-SIASA

Raila Odinga ataka uchaguzi mwengine kufanyika Kenya

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, Raila Odinga.
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, Raila Odinga. REUTERS/Baz Ratner

Kinara wa muungano wa upinzani nchini NASA, Raila Odinga anashinikiza kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya mwezi Agosti mwaka huu lakini pia ametupilia mbali madai kuwa ana mpango wowote wa kuipindua Serikali ya rais Uhuru Kenyatta.

Matangazo ya kibiashara

Odinga amesisitiza kutomtambua Kenyatta kama rais akisema hakupata mamlaka hayo kihalali kutoka kwa wananchi ambapo ameongeza kuwa kama rais wa wananchi atatengeneza mabaraza ya wananchi kujadili mustakabali wao akiweka kando uwezekano wa kuunda baraza lake la mawaziri.

Hayo yanajiri wakati ambapo Serikali ya Kenya ilimfurusha mwanasiasa wa muungano wa upinzani, Nasa, Miguna Miguna na kupelekwa nchini Canada.

Wachambuzi wanasema kuwa inaonekana ni Serikali ya Kenya kutaka kuwanyamazisha wapinzani na kuwashughulikia viongozi walioshiriki kwenye sherehe za kuapishwa kwa kinara wa upinzani Raila Odinga juma moja lililopita.

Miguna Miguna alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais Uhuru Kenyatta.

Katika hatua nyingine jaji mkuu wa Kenya David Maraga hapo jana amevunja ukimya na kuionya Serikali na watu dhidi ya kutoheshimu maelekezo ya mahakama siku chache baada ya Serikali kukaidi kumuwasilisha mahakamani Miguna na mkuu wa jeshi la Polisi kukataa kufika mahakamani.