BURUNDI-HAKI

Kesi ya mwanaharakati wa haki za binadamu Burundi yaombwa kuahirishwa

Polisi wa Burundi baada ya mashambulizi ya grunedi, Bujumbura mnamo Februari 15, 2016.
Polisi wa Burundi baada ya mashambulizi ya grunedi, Bujumbura mnamo Februari 15, 2016. REUTERS/Evrard Ngendakumana

Wanasheria wa Germain Rukuki, mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Burundi, wameomba kuahirishwa kwa kesi ya mteja wao inayosubiriwa na watu wengi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Alifungwa tangu Julai 13, 2017, akishutumiwa "kujaribu kuhatarisha usalama wa nchi " na "uasi" kwa kushirikiana na shirika la haki za binadamu la Acat-Burundi, ambalo lilipigwa marufuku nchini Burundi kama mashirika mengi ya haki za binadamu nchini humo. Mwendesha mashitaka aliongeza makosa mapya kataika kesi hiyo - mauaji, uharibifu wa mali ya umma, jaribio la kupindua utawala uliochaguliwa kidemokrasia, makosa ambayo upande wa utetezi haukuweza kufahamishwa. Hali hiyo imepelekea wanasheria wa mwanaharakati huyo kuomba kesi inayomkabili mteja wao iahirishwe.

Kwa mujibu wa kiongozi wa Acat-Burundi, Army Niyongere, amesema anashangazwa na kesi ya mfanyakazi wake. Amebaini kwamba viongozi serikalini wanaamini kwamba wanaharakati wa haki za binadamu waliosalia nchini wamekua wakitoa taarifa kwa wenzao walio uhamishoni

Wanadiplomasia waliotaka kuhudhuria kesi hiyo walikataliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International linabaini kwamba kesi inayomkabiliwa Bw Rukuki na ile inayo wakabili wenzake wanne au wanaharakati wa zamani waliofuatiliwa katika kesi zingine inaonyesha utayari wa serikali ya Bujumbura kukandamiza anayethubutu kuikosoa.