TANZANIA-SIASA-UCHAGUZI

Rais Magufuli aagiza uchunguzi wa mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu nchini Tanzania

Rais wa Tanzania, John Magufuli
Rais wa Tanzania, John Magufuli REUTERS/Sadi Said

Rais wa Tanzania John Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Tanzania kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watu wote waliohusika kusababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT, Akwilina Akwiline

Matangazo ya kibiashara

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma shahada ya kwanza ya manunuzi na ugavi alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya basi dogo jijini Dar es salaam, Ijumaa Februari 16 wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chama kikuu cha upinzani Chadema waliokuwa wakiandamana kushinikiza mawakala wao kupewa barua za utambulisho wa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kinondoni.

"Nimesikitishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilini wa Chuo cha Usafirishaji (NIT). Natoa pole kwa familia,ndugu,wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huu. Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili," Rais Magufuli ameandika kupitia mtandao wa Twitter.

Jeshi la polisi tayari linawasikilia kwa mahojiano askari sita ambao walihusika katika oparesheni ya kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku moja kabla ya uchaguzi mdogo.

Katika hatua nyingine mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania kupitia mwenyekiti wake Abdul Nondo umemtaka waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji juu ya suala hilo.