RWANDA-DRC-USALAMA

Wakimbizi wa DRC wakabiliana na askari wa Rwanda

Wakimbizi wa DRC wanapanda basi ili kurudi nyumbani tarehe 6 Agosti 2011, Tchibanga, kusini mwa Gabon.
Wakimbizi wa DRC wanapanda basi ili kurudi nyumbani tarehe 6 Agosti 2011, Tchibanga, kusini mwa Gabon. XAVIER BOURGOIS / AFP

Wakimbizi wa DRC walio katika kambi ya kiziba wilayani karongi magharibi mwa Rwanda wamepambana na jeshi la Rwanda RDF na wakimbizi wawili walipelekwa hospitali baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yamejiri wakati ambapo wakimbizi hao walikuwa njiani kuelekea katika ofisi za UNHCR ili iwasaidie kurudi kwao DRC kwa sababu ya njaa kali kambini.

Vurugu hizo zimetokea baada ya wakimbizi zaidi ya elfu tatu kufungasha virago vyao na kuelekea katika ofisi za Shirika la Wakimbizi duniani UNHCR tawi la Rwanda mjini Karongi Magharibi mwa Rwanda ili shirika hilo liwasaidie kurudi kwao kwani nchini Rwanda wanadai kukabiliwa na njaa kali.

Katika mahojiano na mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya RFI mjini Kigali, Bonaventure Cybahiro, wakimbizi hao wamesema kuwa jeshi la ulinzi na polisi ya Rwanda waliwazuwia njiani na kuwapiga risasi nao wakalazimika kuwarushia mawe.

Takribani wakimbizi elfu tatu walikuwa tayari wamezingira ofisi za Shirika la Wakimbizi Duniani wilayani Karongi. Lakini Polisi wakilua wametumwa katika eneo hilo mapema kabla ya maandamano hayo.

Sababu inayowafanya wakimbizi hao kurudi nyumbani ni tatizo la njaa pamoja na kukwepa kuwa Wanyarwanda kwani wamedai kuwa, serikali ya Kigali inataka kuwapa uraia kwa nguvu.

Waziri wa majanga na wakimbizi Bi De Bonhuer Jeanne d’Arc amesema serikali ya Rwanda haina mpango wa kuwapa uraia na hawawezi kufanya hivyo kwa mtu ambaye hajaomba kuwa Mnyarwanda.

"Hilo haliwezekani ili mtu awe mnyarwanda kuna utaratibu wa kufuatwa na kuhusu hilo la kuwapiga risasi kusema kweli taarifa hizo hatujazisikia, lakini hata hivyo, watu wa usalama hawawezi kufumbia macho watu wanaotoka kambini bila utaratibu, " amesema waziri.