SUDANI KUSINI-USALAMA

Maafisa 40 wa jeshi washtumiwa uhalifu wa kivita Sudan Kusini

Askari wa Sudan Kusini.
Askari wa Sudan Kusini. REUTERS/Jok Solomun

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema leo Ijumaa kuwa wamewatambua zaidi ya maafisa 40 wa kijeshi la Sudan Kusini ambao walihusika kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Sudan Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Katika siku za nyuma, Umoja wa Mataifa ulilaani uhalifu mkubwa uliotekelezwa nchini humo, na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Desemba 2013, miaka miwili baada ya uhuru wa nchi hiyo, lakini hii ni mara ya kwanza ripoti ya Umoja wa Mataifa kutaja wahusika wa uhalifu huo.

Machafuko nchini Sudan Kusini, nchi yenye utajiri wa hidrokaboni, yalisababishwa na tofauti kati ya Rais Salva Kiir, kutoka jamii ya Dinka, na Makamu wake, Riek Machar, kutoka jamii ya Nuer. Watu zaidi ya milioni nne, sawa na theluthi moja ya raia wa nchi hiyo, wamelazimika kuyahama makazi yao kufuatia machafuko hayo.

Wachunguzi kutoka Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini wamesema kuwa matokeo ya kazi yao yanatokana na mahojiano kutoka kwa mashahidi zaidi ya mia moja kwenye picha za satelaiti na kwa nyaraka karibu 60,000 za tangu kuanza kwa vita nchini Sudana Kusini.

Ripoti yao, iliyotolewa leo Ijumaa, inasema uhalifu huo ulitekelezwa na kila mmoja kati ya maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa maafisa nane wa cheo cha juu zaidi, na magavana watatu wa majimbo. .

Msemaji wa serikali amesema serikali iko tayari kumuweka jela yeyote aliyehusika na uhalifu.

"Serikali itamfikisha mahakamani mtu yeyote menye hatia, hii ni serikali thabiti inayotekeleza majukumu yake," msemaji wa wizara ya mambo ya nje ameliambia shirika la habari la Reuters.