BURUNDI-MAZUNGUMZO-EAC

Mazungumzo ya kisiasa ya Burundi kuendelea

Makamu wa rais wa kwanza wa Burundi  Gaston Sindimwo akiwa katika mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Februari 23 2018 jijini Kampala nchini Uganda
Makamu wa rais wa kwanza wa Burundi Gaston Sindimwo akiwa katika mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Februari 23 2018 jijini Kampala nchini Uganda Gaël Grilhot/RFI

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanataka pande zote zinazotofautiana nchini Burundi kuendelea na mazungumzo ya kisiasa ili kupata mwafaka.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hii imekuja baada ya viongozi hao kupokea ripoti kuhusu mazungumzo kutoka kwa mratibu wa mazunngumzo hayo rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa.

Alain-Aimé Nyamitwe Waziri wa Mambo ya nje wa Burundi akizungumza na mwandishi wa RFI jijini Kampala Charlotte Cossey, amesema mazungumzo hayo yataendelea ili kupata mwafaka.

“Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamekubaliana kuwa mazungumzo ya Warundi yaendelee yakiratibiwa na rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa.

Aidha, Nyamitwe amekanusha madai ambayo yamekuwa yakisambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa mratibu wa mazungumzo hayo rais wa zamani wa Tanzania Mkapa amejiuzulu.

“Mmekuwa mkisoma kupitia mitandao ya kijamii kuwa mratibu wa mazungumzo haya rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa amejiuzulu, hii si kweli,” aliongeza.

Mazungumzo ya kisiasa ya Burundi yalikuja baada ya mzozo wa kisiasa mwaka 2015 wakati rais Piere Nkurunziza alipowania urais kwa muhula wa tatu kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Wanasiasa wa upinzani chini ya muungano wa CNARED ambao wanaishi nje ya nchi, wamekuwa wakishiriki au wakati mwingine kususia mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakifanyika mjini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.