TANZANIA-HABARI-

Kampuni ya Mwananchi yalalama kutoonekana kwa mwandishi wake kwa siku 100

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai akizungumza Jijini Dar es Salaam, 28 Februari 2018
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Francis Nanai akizungumza Jijini Dar es Salaam, 28 Februari 2018 Fredrick Nwaka/RFI

Kampuni ya Mwananchi Communications Limited imeeleza kusikitishwa na hatua ya kutoonekana kwa mwandishi wake Azory Gwanda aliyetoweka siku 100 zilizopita katika Wilaya ya Kibiti Mkoani, Pwani.

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Francis Nanai amewaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kwamba licha ya kampuni yake kusikitishwa na kutoonekana kwa mwandishi wake bado ina imani na vyombo vya usalama na kuwataka wadau wengine kusaidiana na kampuni yake kumsaka mwandishi huyo.

Azory Gwanda alitoweka Desemba, 7 mwaka 2017 na kutoonekana kwake kumezua wasiwasi miongoni mwa wadau wa tasnia ya habari nchini Tanzania.

Baadhi ya waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wameiambia idhaa ya kiswahili ya RFI kwamba wanafanya kazi kwa wasiwasi na hofu.

Waandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, 28 Februari 2018
Waandishi wa habari wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, 28 Februari 2018 Fredrick Nwaka/RFI

Hata hivyo, wiki kadhaa zilizopita jeshi la polisi nchini Tanzania liliarifu kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine ,Mwenyekiti wa mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania Onesmo Ole Ngurumwa ameonya kuwa huenda matukio hayo yakaendelea ikiwa vyombo vya usalama havitakuwa makini kushughulikia matukio yanayohatarisha usalama wa taifa.