KENYA-KATIBA-SIASA

Mswada unaopendekeza Waziri Mkuu mwenye mamlaka nchini Kenya wapelekwa bungeni

Bunge la Kenya
Bunge la Kenya www.voanews.com

Mbunge wa chama cha KANU nchini Kenya Kassait Kamket, amependekeza mswada bungeni unaolenga kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo kwa kuibadilisha Katiba.

Matangazo ya kibiashara

Mswada huu iwapo utakubaliwa na wabunge, ina maana kuwa Katiba mpya ya Kenya iliyopatikana mwaka 2010, itafanyiwa mabadiliko makubwa.

Mbunge huyo anapendekeza kuundwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu atakayekuwa na madaraka makubwa lakini pia kuwepo kwa rais ambaye atakuwa ishara ya umoja wa kitaifa.

Iwapo marekebisho hayo yatafanyika, bunge la pamoja, lile la kitaifa na Senate litamchagua rais ambaye atakuwa na jukumu la kumteua Waziri Mkuu kutoka kwenye chama chenye wabunge wengi bungeni.

Waziri Mkuu atahudumu kwa muda wa miaka mitano kabla ya Uchaguzi mwingine kufanyika, huku rais ambaye ni lazima awe na zaidi ya miaka 50, akihudumu kwa muhula mmoja wa miaka saba.

Hatua hii imeanzisha mjadala ambao umekuwepo kwa muda mrefu nchini humo, kuhusu mfumo sahihi wa uongozi utakaomaliza mzozo wa kisiasa nchini humo.

Wanasiasa wa upinzani na viongozi wa dini wamekuwa wakisema mfumo huu ndio utakaosaidia kumaliza mvutano wa kihistoria wa kisiasa hasa kuhusu wadhifa wa urais.