Rwanda yatetea uamuzi wake wa kufunga makanisa na Msikiti

Waumini washiriki misa katika Kanisa la Sainte-Famille, Kigali, Aprili 6, 2014.
Waumini washiriki misa katika Kanisa la Sainte-Famille, Kigali, Aprili 6, 2014. REUTERS/Noor Khamis

Serikali ya Rwanda imetetea uamuzi wake wa kuyafunga makanisa 714, operesheni ambayo ilianza wiki moja iliyopita. Rwanda inasema sehemu hizo za ibada hazijatimiza masharti yaliyowekwa.

Matangazo ya kibiashara

Mamlaka ya Rwanda ilitangaza Jumatano jana kuwa makanisa hayo 714 na Msikiti mmoja lazima yafunge milango katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali kwa kukosa kutimiza masharti yaliyowekwa ya usafi na usalama.

Hata hivyo chanzo kimoja cha serikali kimesema viongozi wa makanisa ambayo yamefungwa wamepewa muda wa kutafakari kuhusu namna ya kuheshimu utaratibu uliowekwa na serikali kwenye mji huo, kwa kutimiza masharti ya viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa.

Mkuu wa kamati ya kuyatathmini mashirika ya umma na ya kibinafsi Anastase Shyaka, amesema baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya kazi kwa kutumia mahema na miundombinu chafu, hayana maeneo ya kutosha ya kuegesha magari ya waumini wala vyoo safi.

Shyaka amesema wengi baadhi ya viongozi wa makanisa hayo hawana elimu ya theolojia.

Kuanzia sasa makanisa haya yametakiwa kuwasilisha upya maombi ya leseni ili yaruhusiwe kuendelea kufanya kazi za ibada, amesema afisa huyo wa serikali ya Rwanda.