TANZANIA-MAREKANI-EU

Tanzania yakanusha ripoti ya EU na Marekani kuhusu haki za binadamu na usalama

Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Augustine Mahiga
Waziri wa Mambo ya nje wa Tanzania Augustine Mahiga rfi k

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa imejibu matamko yaliyotolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya hivi karibuni kuhusu mwenendo wa usalama nchini.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Ulaya (EU) hivi karibuni ulitoa tamko lililoelezea kusikitishwa na mauaji ya mwanafunzi wa chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji NIT Akwline Akwilini, aliyepoteza maisha kwa kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu, wakati polisi ikitawanya wafuasi wa upinzani.

Katika tamko hilo Umoja wa Ulaya ulikaribisha wito wa Rais John Magufuli wa kufanyika uchunguzi wa kifo hicho na vifo vingine vya wanaharakati na wanasiasa vilivyotokea hivi karibuni.

Nao Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa tamko la kulaani mauaji ya kiongozi wa Chadema wa kata ya Hananasifu Daniel John na kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa wazi.

Amesema nchi hizo washirika hazitambui changamoto za kiusalama na kisiasa ambazo Tanzania imezipitia kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Mahiga amesema nchi hizo washirika zinapaswa kufuatilia na kuripoti matukio ya kiusalama na kisiasa kwenye nchi zao.

“Hawa wageni na wanadiplomasia wanapaswa kuweka jitihada za kufahamu mazingira magumu yaliyopo nchini badala ya kutoa matamko ya hisia na yasiyothibitishwa ambayo yanaweza kuwa ya kichochezi kwa umma,”amesema Dr Mahiga.

Aidha Waziri Mahiga amesema serikali ya Tanzania ilishangazwa na ukimya wa wanadiplomasia hao wakati wa vitisho vya kiusalama na changamoto ambazo Tanzania ilipitia wakati wa mauaji ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Katika taarifa hiyo Dr. Mahiga alisema msimamo wa serikali ya Tanzania ni kuhifadhi taswira ya taifa na kwamba inakaribisha mazungumzo na wanadiplomasia hao kwa mambo wanayohitaji ufafanuzi ili wafahamu hali halisi.