BURUNDI-SIASA-NKURUNZIZA

Chama tawala nchini Burundi chafafanua cheo kipya alichopewa rais Nkurunziza

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima hivi karibuni
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akikagua gwaride la heshima hivi karibuni REUTERS/Evrard Ngendakumana

Chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD kimefafanua kuwa cheo cha "Imboneza yamaho", kwa lugha ya Kirundi alichopewa rais Pierre Nkurunziza hakina maana kuwa atasalia kiongozi wa chama hicho milele.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa chama hicho Evariste Ndayishimiye ameeleza kuwa cheo hicho kina maana kuwa rais Nkurunziza ndiye mbeba maono ya chama hicho wala sio kama inavyoripotiwa kuwa ataendelea kuwa kiongozi wa chama hicho milele.

“Baada ya kazi kubwa aliyofanya na Mheshimiwa rais, tulibaini kuwa anastahili kuwa kiongozi anayestahili kuendelea kutupa mwelekeo, ushauri na kuendelea kubeba maoni ya chama chetu,” alisema.

Hata hivyo, wakosoaji wa rais Nkurunziza wanasema cheo hicho kina maana kuwa ataendelea kusalia madarakani milele.

Nkurunziza aliingia madarakani mwaka 2005 na kutokana na mchakato wa kuibadilisha Katiba unaoendelea , rais huyo anatarajiwa kuwania tena urais mwaka 2020 na kuendelea madarakani hadi mwaka 2034 na hatimaye muda wote wa uhai wake.