TANZANIA-SIASA-USALAMA

Tundu lissu-Bado sijafahamu lini nitarejea Tanzania

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, akizungumza na Wanahabari katika hosoitali ya Nairobi nchini Kenya Januari 05 2018
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu, akizungumza na Wanahabari katika hosoitali ya Nairobi nchini Kenya Januari 05 2018 www.mwananchi.co.tz

Mwanasiasa wa upinzani na mwanasheria Mkuu wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu anatarajiwa kufanyiwa oparesheni ya nyingine ya mguu wiki ijayo ikiwa ni oparesheni ya 20 tangu alipopigwa risasi Septemba mwaka jana akiwa mkoani Dodoma.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na Idhaa ya kiswahili ya RFI kutoka nchini Ubelgiji mwanasiasa huyo ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki amesema ni mapema kujua lini atarejea nchini Tanzania kuendelea na shughuli za kisiasa.

“Ninaendelea vizuri na matibabu, niliumizwa sana sehemu mbalimbali na mwili na hsa mguu wa kulia. Tangu nimekuja hapa Ubelgiji nimefanyiwa oparesheni mbili na imebaki moja. Hivyo siwezi kujua itachukua muda gani na sifahamu lini nitarejea nyumbani,”amesema kiongozi huyo ambaye pia ni mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani katika bunge la Tanzania.

Kiongozi huyo amesema baada ya kufanyiwa oparesheni nyingine wiki ijayo ataendelea na mazoezi ya viungo ili kuimarisha mwili wake.

Kabla ya kuelekea nchini Ubelgiji kwa matibabu Lissu alipata matibabu kwa miezi minne katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na kabla ya kuondoka nchini humo alisema shambulio dhidi yake lilikuwa ni sawa na mauaji ya kisiasa.