BURUNDI-KATIBA-SIASA-USALAMA

Kura ya maoni Burundi: Upinzani watakiwa kuwasilisha malalamiko yake CENI

Kiongozi wa muungano wa Amizero y'Abarundi, Agathon Rwasa, akishiriki zoezi la kupiga kura kuhusu mabadiliko ya Katiba katika kituo cha kupigia kura cha Kiremba, Ngozi, Mei 17, 2018.
Kiongozi wa muungano wa Amizero y'Abarundi, Agathon Rwasa, akishiriki zoezi la kupiga kura kuhusu mabadiliko ya Katiba katika kituo cha kupigia kura cha Kiremba, Ngozi, Mei 17, 2018. REUTERS/Evrard Ngendakumana

Serikali ya Burundi imewataka wanasiasa wa upinzani nchini humo kutumia njia za kisheria kuwasilisha malalamiko yao kupinga matokeo ya kura ya maoni yaliyotangazwa juma hili ambapo wananchi waliunga mkono kufanyika kwa marekebisho ya katiba ambayo huenda yakashuhudia rais Pierre Nkurunziza akisalia madarakani hadi mwaka 2034.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani umesisitiza kuwa hautambui matokeo yaliyotangazwa Jumatatu ya wiki hii ambapo umedai kura iliyofanyika haikuwa huru na haki huku wafuasi wake wengi wakitishiwa na wengine kuuawa wakati wa kipindi cha kampeni.

Akizungumza na idhaa ya RFI Kiswahili, balozi wa Burundi nchini Tanzania Gervais Abayeho amesema mchakato uliofanyika ulifuata taratibu za kisheria na kuwataka wanaopinga kuwasilisha malalamiko yao kwa tume ya uchaguzi CENI.

Haya yanajiri wakati huu matokeo yaliyotangazwa yanasubiriwa kuthibitishwa na mahakama ya katiba.

Marekebisho yaliyoibua sintofahamu ni kuhusu muhula wa rais ambapo ikiidhinishwa kutakuwa na kipindi cha miaka 7 tofauti na mfumo wa sasa wa miaka mitano kwa mihula miwili.