KENYA-UHURU

Kenya yaadhimisha miaka 55 ya uhuru wake

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa sherehe za madaraka day.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa sherehe za madaraka day. Kenyagvt

Kenya inaadhimisha miaka 55 ya Madaraka. Siku kama ya leo mwaka 1963, baada ya mapigano ya miaka mingi dhidi ya wakoloni kutoka Uingereza, Kenya ilijihakikishia uhuru wake kuelekea kuwa Jamhuri kamili.

Matangazo ya kibiashara

Wakati taifa la Kenya likiadhimisha makala ya 55 ya Madaraka Dei leo Ijumaa na ambapo hafla rasmi ni katika uwanja wa Kinoru, Kaunti ya Meru, baadhi ya manusura wa vita vya kukomboa taifa hilo kutoka minyororo ya ukoloni wanasema kuwa Kenya haijapiga hatua katika nyanja mbalimbali.

Hata hivyo wanasema mengi ni yale yamebakia kuwa ndoto tu huku taifa likiwa kwa sasa limezama ndani ya dimbwi la ufisadi mkuu.

Maveterani hao wamekosoa utawala wa rais Kenyatta wakiulinganisha na tawala zilizotangulia.

“Kenyatta anaonekana wazi kufuata nyayo za serikali zilizotangulia ambapo hazikutambua mashujaa wa nchi kikamilifu, “ wamesema baadhi ya maveterani wakihojiwa na shirika la habari la AFP, huku wanamtaka atekeleze vita mpya vya ukombozi dhidi ya ufisadi wa rasilimali za Wakenya ili ndoto ya uhuru halisi itimie.

Mwenyekiti wa Maumau Veterans Association (MVA) Gitu Kahengeri amesema: "Kupenda nchi yetu ni kuongea ukweli unaouma kuhusu maisha ya Wakenya kwa kuwa ndio wenye nchi. Hakuna haja ya kusombwa na kasumba za ubinafsi kiasi cha kusisitiza tunafaa kucheka wakati tunafaa kuwa katika hali ya majonzi."

Kahengeri amebaini kuwa hakuna ustaarabu wa uongozi ndani ya miaka 55 baada ya uhuru, wakat i ambapo kilo moja ya unga kwa masikini inanunuliwa bei ya Shilingi za Kenya 110.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Central Kenya Maumau Association (CKMA) Joram Gichuki, kinyume na ndoto yao ya awali ya kupigania uhuru wa kujitawala, vita dhidi ya changamoto hizo nyeti vilikwama.

Gichuki anasema kuwa hali hiyo imechangiwa pakubwa na sera zisizo thabiti za kulainisha uongozi wa taifa, mbali na sera nyingi ambazo zimekuwa za kukimbizana na manufaa ya kibinafsi huku viongozi wakiungana na igogo matapeli kujitajirisha zaidi na hivyo kufukarisha Mkenya wa kawaida.