TANZANIA-JOHN MAGUFULI

Viongozi waandamizi wa serikali, kuhudhuria mazishi ya mapacha walioungana Tanzania

Maria na Consolata, pacha waliofariki dunia jana Mkoani Iringa
Maria na Consolata, pacha waliofariki dunia jana Mkoani Iringa Mwananchi

Serikali Mkoani Iringa, Kusini Magharibi mwa Tanzania imesema mazishi ya mapacha walioungana Maria na Consolata yatafanyika Jumatano katika makaburi ya Tosamaganga Mkoani humo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali.

Matangazo ya kibiashara

Maria na Consolata, mapacha pekee walioungana walifariki dunia juzi wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Richard Kasesela, Mkuu wa Wilaya ya Iringa ameiambia RFI Kiswahili kuwa waziri wa elimu, Profesa Joyce Ndalichako na naibu waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Stella Ikupa ni miongoni mwa waombolezaji wanaotazamiwa kushiriki mazishi ya mabinti hao.

“Kabla ya mazishi siku ya Jumatano, kutakuwa na misa ya wafu itakayofanyika Chuo Kikuu cha kikatoliki cha Ruaha hapa Iringa na baadaye kuelekea Tosamaganga kwa mazishi. Tunatarajia kuwa na Waziri wa elimu Profesa Ndalichako na viongozi wengine,”amesema kiongozi huyo.

Mahala watakapozikwa mabinti hao, waliokuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, hutumiwa pia kwa mazishi ya mapadri na masista.

Maria na Consolata walifariki walizaliwa mwaka 1996 katika Hospitali ya misheni ya Ikonda iliyopo Makete, Mkoani Njombe na hadi wanakutwa na mauti walikuwa wakitunza na kulelewa na shirika la masista wa Maria consolata.