SUDANI KUSINI-SIASA-USALAMA

Wabunge waanza mjadala kuhusu mageuzi ya katiba Sudan Kusini

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir. REUTERS/Jok Solomun

Wabunge nchini Sudan Kusini wameanza mjadala wa kuibadilisha Katiba, ili kumruhusu rais Salva Kiir kuendelea kuongoza kwa muda wa miaka mitatu zaidi.

Matangazo ya kibiashara

Iwapo mabadiliko hayo yatafanyika, rais Kiir pamoja na wasaidizi wake na wabunge, wataendelea kuwa mamlakani hadi mwaka 2021.

Mwaka 2015, bunge lilipitisha mswada wa kumruhusu rais Kir kuongoza kwa miaka mitatu zaidi.

Haya yanajiri wakati ambapo Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Mouusa Faki, anataka hatua kuchuliwa dhidi ya viongozi wa juu wa Sudan Kusini wanaosababisha kuvunjika kwa mkataba wa amani.

Kauli ya Faki, imekuja baada ya waasi nchini Sudan Kusini kuishtumu serikali kuvunja mkataba wa kusitisha mapigano ambao ulianza kutekelezwa siku ya Jumamosi.

Mkuu huyo wa AU, amesisitiza kuwa, huu ni wakati wa kuchukua hatua kwa sababu, viongozi wa Sudan Kusini wamekuwa na tabia ya kutoheshimu mikataba ya amani wanayokubaliana kutekeleza.

Wiki hii rais Salva Kiir na hasimu wake, Riek Machar walikubaliana kusitisha mapigano kabisa ndani ya saa 72, baada ya kukutana jijini Khartoum nchini Sudan, lakini utekelezwaji wa makubaliano hayo, upo mashakani.

Mapigano nchini Sudan Kusini yamekuwa yakiendelea kwa tangu mwaka 2015, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kuyakimbia makwao.

Raia wa Sudan Kusini waliobaki nyumbani, wanakosa huduma muhimu kama chakula, maji safi na dawa na utekelezwaji wa mkataba wa amani ndio tumaini lao kuwa kutakuwa na utulivu.