TANZANIA-SIASA-CHADEMA-CCM

Mbunge wa upinzani Tanzania, atimkia chama tawala huku akishutumu upinzani

Aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara akitangaza kujiunga na CCM, Julai 28 mwaka 2018 jijini Dar es Salaam
Aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara akitangaza kujiunga na CCM, Julai 28 mwaka 2018 jijini Dar es Salaam Instagram/Kwanza TV

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Mwita Waitara ametangaza kujiengua katika chama kikuu cha upinzani cha chadema na kujiunga na Chama tawala, CCM.

Matangazo ya kibiashara

Waitara aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga lililopo Dar es salaam amefikia uamuzi huo leo katika mkutano na wanahabari uliofanyika makao makuu madogo ya CCM, Lumumba huku akishutumu chama alichotoka, Chadema, kuwa hakina demokrasia na pia kotofautiana na mwenyekiti wa chadema Freeman Mbowe.

Aidha amesema chama hicho kikuu cha upinzani kimeshindwa kujenga ofisi  ya kitaifa na ofisi za kanda licha ya kupokea ruzuku inayozidi milioni 200 kila mwezi.

Waitara ambaye kwenye mkutano huo aliambatana na Katibu mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole amekisifia chama tawala na viongozi wake kwa kudai wanaokwenda spidi katika kuwatumikia watanzania.

"Chadema ni kampuni na sio taasisi, ukiwa nje unaweza kudhani ni makamanda kweli lakini ukiingia ukaona yanayofanyika ni shida,"amesema Waitara

Awali, Waitara aliitumikia CCM kutoka mwaka 1998 hadi 2008 alipong'oka na kujiunga na Chadema.

Kwa mujibu wa sheria mwanasiasa huyo sasa anakuwa amejiengua katika nyadhifa zake za kisiasa ikiwemo ubunge aliopata mwaka 2015.

Baadhi ya viongozi wa chama tawala na wafuasi wao wamemiminika kwenye mitandao ya kijamii, wakipongeza uamuzi wa Waitara huku wanasiasa wa upinzani wamimshutumu kwa usaliti.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini Tanzania, wanasiasa wa upinzani wakiwemo wabunge na madiwani wamekuwa wakijuzulu nyadhifa zao na kujiunga na Chama tawala, kwa wanachodai kuuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano.

Kujiuzulu kwa wanasiasa hao kumepelekea serikali kutumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kugharamia uchaguzi wa marudio katika maeneo mbalimbali nchini.