BURUNDI-USALAMA

Askari watatu wauawa katika shambulio kaskazini mwa Bujumbura

Askari wa Burundi wakipiga doria karibu na msitu wa Rukoko.
Askari wa Burundi wakipiga doria karibu na msitu wa Rukoko. AFP / Esdras Ndikumana

Askari watatu wa Burundi waliuawa na wengine watano walijeruhiwa mapema wiki hii katika shambulio la kuvizia katika msitu wa Rukoko, kilomita kumi na tano kutoka Bujumbura.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa muungano wa waandishi wa habari nchini humo (SOS Media Burundi), shambulizi hilo lililoendeshwa dhidi ya gari la jeshi lilitokea karibu saa nne usiku siku ya Jumapili kuamkia Jumatatu wilayani Gihanga katika mkoa wa Bubanza.

"Gari lililokua limebeba askari kadhaa ambalo limekua likielekea katika ngome ya jeshi katika msitu wa Rukoko lilishambuliwa kwa risasi na kundi la watu wenye silaha wasiojulikana", chanzo cha polisi ambacho hakikutaja jina lake kimeliambia shirika la habari la AFP.

"Askari watatu waliuawa papo hapo na wengine watano walijeruhiwa, ambapo watatu wako katika hali mbaya," chanzo hicho kimesema, na kuongeza kuwa washambuliaji "walitoweka msituni baada ya shambulizi hilo."

Serikali haijathibitisha shambulio hilo, lakini mashahidi wanasema kuwa shambulio hilo lilitokea katika msitu wa Rukoko kwenye mpaka na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo kundi la waasi la FNL linaloongozwa na Jenerali Aloys Nzabampema, limesema kuwa limehusika na shambulizi hilo.