Kampeni ya kuhifadhi mazingira yaanza, majengo ya kifahari yaangushwa
Shirika la kitaifa la kuhifadhi Mazingira nchini Kenya NEMA, limeanza zoezi la kubomoa majengo yote yaliyojengwa karibu na maeneo ambayo kuna mito au vyanzo vya maji.
Imechapishwa:
Zoezi hili limeanzia katika jiji kuu la nchi hiyo Nairobi, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa ulinzi.
Siku ya Jumanne na Jumatano, wafanyibiashara katika majengo makubwa hasa duka la jumla la Southend pembezoni mwa barabara ya Lang'ata waliamka na kupata jengo hilo likiendelea kubomolewa.
Licha ya malalamishi kutoka kwa wamiliki wa majengo hayo na wafanyibiashara kuwa wameharibiwa mali zao.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMA Profesa Geoffrey Wahungu, amesema Shirika hilo lilitoa taarifa mapema kwa wahusika wote kabla ya kuanza kutekeleza ubomoaji huo.
Majengo ya kifahari, kituo cha mafuta na Mkahawa unaozuwa Kahawa maarufu kama Java House katika mtaa wa kifahari wa Kileleleshwa ni miongoni mwa majengo yaliyobomolewa kwa sababu ya kujengwa pembezoni mwa Mto Nairobi.
Kumekuwa na maandamano kupinga ubomoaji huu, ambao serikali inasema itasaidia katika kuhifadhi mazingira na kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.