SOKA-CECAFA-AFCON

Mechi za kufuzu fainali za Afrika kwa vijana zaanza Dar

Nembo ya fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, zitakazochezwa mwaka 2019 nchini Tanzania
Nembo ya fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, zitakazochezwa mwaka 2019 nchini Tanzania wikipedia

Mechi za kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zinaanza leo nchini Tanzania zikishirikisha mataifa tisa kutoka ukanda wa Cecafa. Mchezo wa awali utakuwa kati ya Rwanda na Sudan Saa 8:00 kabla ya wenyeji, Tanzania kumenyana na Burundi Saa 11:00 jioni na kiingilio ni bure.

Matangazo ya kibiashara

Shirikisho la Soka barani Afrika, lilibadili utaraibu mpya wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali hizo ambapo kwa  sasa mechi za kufuzu zinachezwa kwenye kanda mbalimbali badala ya utaratibu wa awali ambapo nchi kutoka kanda moja zilikuwa zikishindana na nchi kutoka ukanda mwingine.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali hizo mwakani na tayari nchi shiriki zimewasili nchini humo kwa michezo hiyo ya kufuzu ambayo itachezwa uwanja wa Taifa na Uwanja wa Chamazi.

Nchi tisa za Afrika Mashariki na kati zikiwemo Kenya, Tanzania na Rwanda zinashiriki michuano hiyo itakayofikia tamati Agosti 26 ambapo ukanda wa Cecafa utatoa nchi mbili.

Tayari dosari za wachezaji kuzidi umri zimejitokeza ambapo CAF ililazimika kuwaondoa baadhi ya wachezaji kushiriki michuano hiyo.

Taarifa ya Makamu wa Rais wa Kamati ya Tiba ya CAF, Dk Yacine Zerguini imewataja wachezaji wengine walioenguliwa ni Abdoul Intwari wa Burundi, Maxwell Mullili, Lesley Otieno na Abdulmalik Hussein Abdallah wa Kenya, Simon Pitia Alberto wa Sudan Kusini, Gamel Abdou Kamal wa Sudan, Oluka George, Kafumbe Joseph na Elvis Ngonde wa Uganda.