Dereva wa mbunge Bobi Wine auawa Uganda
Imechapishwa:
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda na mwanamuziki Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amedai kuwa polisi wamempiga risasi na kumuua dereva wake.
Mauaji hayo yalitokea wakati wa kumalizika kwa kampeni za kisiasa Jumatatu jioni kuelekea uchaguzi mdogo bunge wa eneo la Arua, siku ya Jumatano.
Mwanasiasa huyo maarufu anayeongoza vuguvugu la People'a Power, amesema polisi walimlenga wakati alipokuwa anamnadi mgombea wa vuguvugu hilo.
“Polisi wamempiga risasi na kumuua dereva wangu, walifikiri wameniua,” amesema mbunge huyo wa jimbo la Kyadondo.
Msemaji wa Polisi Emirian Kayima amekataa kuzungumzia madai hayo, wakati huu uchunguzi ukiendelea kubaini ukweli wa mambo.
Ripoti zinasema pia kuwa gari la rais Yoweri Museveni lilishambuliwa, wakati alipokuwa anapita katika eneo la jimbo hilo la Arua.