UGANDA-USALAMA-SIASA-HAKI

Bobi Wine na washukiwa wengine 30 kuripoti mahakamani Uganda

Mwanamuziki na Mbunge wa upinzani Robert Kyagulanyi anayefahamika kwa jina la Bobi Wine Alhamisi wiki hii anatarajiwa kuripoti mahakamani huko Gulu, Kaskazini mwa Uganda kusikiliza uamuzi wa mahakama.

Le musicien et politicien Bobi Wine lors d'une manifestation à Kampala, le 11 juillet 2018.
Le musicien et politicien Bobi Wine lors d'une manifestation à Kampala, le 11 juillet 2018. Isaac Kasamani / AFP
Matangazo ya kibiashara

Bobi Wine na washukiwa wenzake thelathini wanakabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Kwa mujibu wa chanzo cha mahakama, Bobi Wine na washukiwa wegine 32 watasomewa mashtaka yao kisha kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu, kwani Mahakama ya mwanzo ya Gulu haina mamlaka ya kisheria kuendesha kesi za uhaini.

Alikamatwa wiki mbili zilizopita kwa tuhuma za uvamizi wa msafara wa Rais Museveni mjini Arua na kupokea kipigo kikali yeye na wenzie 32 kutoka kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Dereva wa Bobi Wine alipigwa risasi na kuuawa katika purukushani hizo.

Awali Bobi Wine alifikishwa katika mahakama ya kijeshi kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria. Lakini Mahaka ya kijeshi ilimuachilia huru baada ya kutomkuta na hatia.

Bobi Wine alikamatwa pamoja na watuhumiwa wengine 33 kufuatia tukio la Arua, kaskazini mwa Uganda. Anashtumiwa kuhusika katika vurugu za kurushia mawe magari ya msafara wa rais Yoweri Kaguta Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Arua.

Mapema wiki hii Jaji Stephen Mubiru, Mkuu wa mahakama ya Gulu (kaskazini), alikubali ombi la Kyagulanyi na baadhi ya watuhumiwa wenzake, ikiwa ni pamoja na wabunge wawili wa upinzani kuachiliwa huru kwa dhamana.

Kyagulanyi, mwenye umri wa miaka 36, ameibuka kama msemaji wa vijana wa Uganda na mpinzani mkuu wa rais Yoweri Museveni tangu uchaguzi wake kama mbunge mnamo mwaka 2017. Kufungwa kwake kulizua maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali nchini Uganda, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Kampala, ambapo polisi ilitumia nguvu kupita kiasi kwa kuzima maandamano hayo.