KENYA-UINGEREZA-USHIRIKIANO-RUSHWA

Waziri Mkuu wa Uingereza aunga mkono vita dhidi ya ufisadi Kenya

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akimpokea rasmi Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May katika ikulu ya State House, Nairobi, Kenya.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akimpokea rasmi Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May katika ikulu ya State House, Nairobi, Kenya. Uhuru Kenyatta (@UKenyatta) | Twitter.html

Uingereza imesema inasimama na Kenya katika kampeni inayoendelea dhidi ya ufisadi, huku ikilenga pia kuimarisha biashara kati ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Matangazo ya kibiashara

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ambaye amezuru Kenya na kufanya mazungumzo na rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, amesema nchi yake inaunga mkono vita dhidi ya ufisadi vinavyoendelea kushuhudiwa.

Kenya na Uingereza zimetia saini mkataba utakaoiwezesha serikali ya Uingereza kurejesha fedha za umma zilizoibiwa na kufichwa nchini Uingereza.

Rais Kenyatta amesema hatarudi nyuma katika vita dhidi ya ufisadi.

Naye Waziri Mkuu May amesema, serikali ya nchi yake itahakikisha hilo linafanyika na nchi yake inasimama na rais Kenyatta katika vita hivyo lakini pia, amefurahishwa na maridhiano ya kisiasa nchini humo.

Wakati viongozi hao wakizungumzia suala la ufisadi, Katibu wa kudumu katika Wizara ya Kilimo Richard Lesiyampe amekamatwa kwa madai ya ufisadi kuhusu sakata la mahindi nchini humo.

Mbali na suala la ufisadi, viongozi hao wawili wametia saini mikataba ya biashara, itakayosaidia ongezeko la ushirikiano wa biashara kati ya Kenya na Uingereza.

Aidha, May amesema, nchi yake itaendelea kuunga mkono vita dhidi ya Al Shabab nchini Somalia na itaongeza kiwango cha fedha kusaidia kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom).

May amezuru Kenya baada ya kutokea Afrika Kusini na Nigeria na anakuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Uingereza kurejea nchini humo ndani ya miaka 30.