UGANDA-USALAMA-SIASA-HAKI

Bobi Wine akamatwa tena, mawakili wake washtumu

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina la Bobi Wine,akifikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Gulu kaskazini mwa Uganda Agosti 23, 2018.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina la Bobi Wine,akifikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Gulu kaskazini mwa Uganda Agosti 23, 2018. STRINGER / AFP

Mwanamuziki na Mbunge wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi anayefahamaiika kwa jina la Bobi Wine anaendelea kuzuiliwa tena katika eneo lisilojulikana kwa mujibu wa wanasheria wake.

Matangazo ya kibiashara

Bobi Wine alikamatwa siku ya Alhamisi wiki hii akiwa anajaribu kuondoka nchini humo kuelekea ughaibuni kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa mwanasheria wake, mbunge huyo alikamatwa jana akiwa uwanja wa ndege licha ya kuwa Mahakama ilimpa dhamana na kuamuru arejeshewe hati yake ya kusafiria.

“Alikamatwa Alhamisi akiwa Uwanja wa Ndege, ingawa jaji aliatoa amri kuwa apewe hati yake ya kusafiria kwa sababu alitaka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu,” amesema mwanasheria wa Bobi Wine, Robert Amsterdam.

Mwanasheria wake Robert Amsterdam anasema kipaumbele cha Bobi Wine ni kupata matibabu na si kuitoroka nchi.

Kabla ya kuzuiliwa kwa Bobi Wine, mbunge mwingine tena wa upinzani Francis Zake pia alizuia Uwanja wa ndege kwa ajili ya kwenda kupata matibabu nje ya nchi.

Bobi Wine alikuwa akishikiliwa na kikosi maalum cha ulinzi wa rais na inadaiwa kuwa alipata maumivu makali kutokana na kipigo.

Kikosi hicho kilimshikilia Bobi Wine pamoja na wabunge wengine wa upinzani kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alishiriki katika vurugu za uchaguzi mdogo ambapo gari la msafara wa Rais lilishambuliwa kwa mawe.

Bobi Wine anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais Yoweri Kaguta Museveni. Aliachiliwa kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa siku ya Jumatatu.