CECAFA-KENYA-SOKA

Kenya yajiondoa kuandaa michuano ya Cecafa

Rais wa Shirikisho la Soka nchini Kenya Nick Mwendwa (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Kenya Nick Mwendwa (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye www.the-star.co.ke

Shirikisho la mchezo wa kandanda nchini Kenya, FKF limetangaza kujiondoa kuandaa michuano ya wanaume kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge Cup) iliyopangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Mwaka jana, taifa hilo lilifanikiwa kuandaa michuano ya Cecafa na kufanikiwa kunyakua taji lakini safari hii Rais wa FKF Nick Mwendwa amesema Kenya haiko tayari kutokana na sababu za kifedha.

"Tumekubali kujiondoa kuandaa michuano ya aina yoyote kwa sasa kutokana na sababu za kifedha, tumeiomba Cecafa kutafuta nchi nyingine itakayoandaa michuano hiyo,"Mwendwa alinukuliwa na vyombo vya habari nchini Kenya.

Taifa hilo lilipewa jukumu la kuandaa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuandaa kwa mafanikio michuano ya mwaka jana.

Mwendwa amesema shirikisho hilo linadaiwa dola laki sita na aliyekuwa kocha wa Harambee Stars Aden Amrouche.

Tayari Shirikisho la Soka Tanzania TFF limesema linafanya tathimini kabla ya kuamua kuandaa michuano ya Cecafa au la.