UGANDA-MUSEVENI-SIASA-USALAMA

Museveni akanusha kuteswa kwa wanasiasa alaumu wanahabari

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni GAEL GRILHOT / AFP

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekanuusha madai ya kuwatesa na kuwapiga wanasiasa na wapinzani na wafuasi wao katika operesehi ya kiusalama hivi karibuni, baada ya kuzuka kwa machafuko Kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Museveni alihotubia taifa kwa zaidi ya saa nne siku ya Jumapili usiku, kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, amevilaumu vyombo vya Habari nchini humo kwa kuripoti taarifa za uongo na kuwapotosha raia.

Amewaelezea wanasiasa wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, kama wanasiasa waliokosa nidhamu na wanaotumiwa na mataifa ya nje.

Bobi Wine ambaye yuko Marekani anakopata matibabu, amekuwa akidai alipigwa na kuteswa na maafisa wa jeshi, baada ya kukamatwa mjini Arua wiki kadhaa zilizopita baada ya msafara wa rais Museveni kurushiwa mawe.

“Mataifa ya kigeni, yanatumia mashirika ya kiraia, kuleta fujo hapa nchini,” alisema Museveni.

“Hatutaruhusu, jiji la Kampala kuharibiwa, eti kijana akichoma tairi la gari analipwa Shilingi Laki Tatu za Uganda,” aliongezea.

Museveni ameyataka Mashirika ya kiraia kupeleka misaada yao ya kifedha katika mataifa yenye uhitaji wa usalama hasa Somalia, badala ya kuwapa vijana wasiokuwa na ajira.

Kuhusu mauaji ya watu wanaopigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwa juu pikipiki, Museveni amelaani mauaji hayo na kusema serikali yake inaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kuna Kamera za siri katika miji ya nchi hiyo, hasa jijini Kampala.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa juu wa jeshi la Polisi Muhammad Kirumira  alipigwa risasi na kuuawa akielekea nyumbani kwake na watu wasiofahamika.

Kabla ya kuuawa kwake, Kirumira alionekana kuwa mkosoaji mkubwa wa jeshi la Polisi chini humo akisema linaongozwa na watu mafisadi na wanaowalinda wahalifu.

Rais Museveni ameahidi kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliohusika.