TANZANIA-NEC-CHADEMA

NEC, Chadema watofautiana, uchaguzi wa majimbo ya Ukonga,Monduli

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania, Jaji Semistocles Kaijage
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania, Jaji Semistocles Kaijage Mwananchi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania NEC na Chama Kikuu cha Upinzani Chadema vimetofautiana kuhusu mwenendo wa uchaguzi katika Jimbo la Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Jimbo la Ukonga, kama ilivyo kwa jimbo la Monduli Mkoani Arusha na kata mbalimbali nchini Tanzania, zinafanya uchaguzi mdogo baada ya waliokuwa wawakilishi wa Majimbo na kata hizo kuvihama vyama vya upinzani na kujiunga na Chama tawala, Chama cha Mapinduzi.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage amenukuliwa na mtandao wa gazeti la Mwananchi akisema uchaguzi huo umekwenda vizuri, baada ya kutembelea vituo kadhaa kikiwemo kituo cha shuel ya msingi Juhudi.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, tanzania Bara, John Mnyika ametuhumu uchaguzi huo  akidai umegubikwa na hujuma.

"Kama mawakala wetu wamenyimwa ruhusua ya kuingia katika vituo vya kupigia kura, tunasikitishwa na kauli ya Jaji Kaijage kuwa uchaguzi unakwenda vizuri. Wananchi watarajie hujuma kwenye uchaguzi huu,"ameeleza Mnyika.

Aidha Mnyika amesema kuna baadhi ya maeneo mawakala wachache waliruhisiwa kuingia ikiwemo kituo cha Kwambunga A, alikodai baadhi ya kura zilikuwa zikipigwa na kuingizwa kwenye vifaa vya kuifadhia kura.

Aidha, habari nyingine zilizochapishwa na mtandao wa Mwananchi zinaeleza kwamba, mgombea wa Chadema katika Jimbo la Monduli, Yonas Laizer amesema mawakala wake kunyimwa fursa ya kuingia kwenye vituo vya kura.

Chama tawala, CCM katika Jimbo la Ukonga kimemsimamisha Mwita Waitara aliyejiunga nacho baada ya kujiengua Chadema wakati Chadema imemsimamisha Asia Msangi.