BURUNDI-UN-HAKI

Burundi kuendelea kuwekewa vikwazo

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza. REUTERS/Evrard Ngendakumana

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi imezitaka nchi wanachama kuendelea kuiwekea vikwazo nchi ya burundi na kuwalenga wahusika wa moja kwa moja na mauaji yanayotajwa katika ripoti ya tume hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Tume hiyo imesema Jumuiya ya Kimataifa haikutekeleza jukumu lake ipasavyo ili kuingilia kati vilivyo kumaliza mzozo wa Burundi.

Hayo ni wakati tume hiyo ikiwasilisha ripoti yake mbele ya baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kilichozinduliwa Jumatatu wiki hii huko Geneva Uswisi ambapo wajumbe wa serikali ambao wapo mjini Geneva wamesusia vikao kuhusu Burundi.

Idadi kubwa ya nchi wanachama wa baraza la haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zimepongeza ripoti hiyo, na kulaani hatuwa ya serikali ya Burundi ya kuwakataza wajumbe wa tume ya uchunguzi kutokanyaga nchini Burundi.

Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Burundi kuanzisha uchunguzi dhidi ya watu waliotajwa ndani ya ripoti, kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Ulaya kwenye baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Stavros Lambrinidis.

Licha ya ripoti hiyo ya tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi kutoyataja majina yote ya wahusika wa mauaji, watu kadhaa wametajwa, wakiwemo waziri wa usalama wa taifa, Alain Guillaume Bunyoni, mkuu wa idara ya upelelezi, mshauri wa rais anaehusika na maswala ya usalama, na yule wa maswala ya kiraia pamoja na katibu mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD, huku rais Nkurunziza akitajwa kuwa ndie anaechochea kupitia hotuba zake.