UGANDA-EU-SIASA

Uganda yaushutumu Umoja wa Ulaya

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni REUTERS/Tiksa Negeri/File Photo

Serikali ya Uganda imelishtumu Bunge la Umoja wa Ulaya kwa kuitaka Mahakama nchini humo kufutilia mbali kesi ya uhaini dhidi ya mbunge wa upinzani, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ambaye yupo nchini Marekani kwa matibabu.

Matangazo ya kibiashara

Bunge hilo, pia lilipitisha azimio na kulaani kuteswa kwa mwanasiasa huyo na wenzake wanaodaiwa kuteswa na maafisa wa usalama, hatua ambayo imekasirisha serikali ya Kampala.

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo amesema serikali imeshangazwa na kauli ya wabunge hao, na kusema walistahili kushinikiza Mahakama kutenda haki badala ya kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.

“Tunalaani, kauli hii ya Umoja wa Ulaya, badala ya kusema Mahakama isikiliza kesi hii na kutenda haki, inajaribu kuingilia Mahakama yetu,” alisema.

Rais Yoweri Museveni amekuwa akiyashtumu mataifa ya nje, kwa kujaribu kuingilia siasa za nchi hiyo na kuongeza kuwa serikali yake haitakubali hilo.

Bobi Wine ambaye hivi karibuni, amejipatia umaarufu hasa  kwa vijana , anatarajiwa kurehea nyumbani baadaye wiki hii baada ya matibabu nchini Marekani.