SIASA-CHADEMA-CCM

Chadema yasusia kushiriki chaguzi ndogo nchini Tanzania

Mwenyekiti wa chama Kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa chama Kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, Freeman Mbowe The Citizen

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimetangaza uamuzi wa kutoshiriki chaguzi zozote ndogo zinazoandaliwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Chama hicho umekuja siku chache baada ya kushindwa na Chama tawala, Chama cha Mapinduzi, CCM katika chaguzi mdogo ziliomalizika wiki iliyopita katika majimbo ya Ukonga Mkoani Dar es Salaam na Monduli Mkoani Arusha sanjari na kata kadhaa nchini humo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman mbowe ameambiwa wanahabari Jijini Dar es Salaam kuwa chama chake kimechukua uamuzi huo kutokana na uvunjifu wa sheria na mifumo ya uchaguzi inayoendelea nchini humo.

"Kwa sasa tunakwenda kufanya mabadiliko ndani ya chama, tunakwenda kujijenga, hatuwezi kushiriki wakati tunaonewa na sheria hazifuatwi.Kwa sasa tunarudi nyuma,"ameeleza Mbowe, mbunge wa kuchaguliwa katika Jimbo la uchaguzi la Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Malalamiko ya Chadema yanakuja wakati ambao Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania ikisema chaguzi ndogo zilizomalizika hivi karibuni ziliendeshwa kikamilifu kwa kuzingatia kanuni na taratibu za uchaguzi.

Tanzania itashuhudia uchaguzi mwingine mdogo katika Jimbo la Liwale, Kusini mwa nchi hiyo baada ya aliyekuwa mbunge wake Mohammed Kuchauka kujiuzulu na kujiunga na CCM ambayo imemteua kuwania ubunge kwenye jimbo hilo.

Aidha kata nyingine 37 zinatarajiwa kufanya chaguzi ndogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya waliokuwa madiwani wake kujiuzulu kwa madai ya kuunga mkono serikali ya rais John Magufuli.

Katika hatua nyingine Mbowe amesema hana mpango wa kujizulu wadhifa wake wa uenyekiti katika chama hicho.