ICC-LRA-UGANDA-ONGWEN

Mawakili wa Ongwen wawataka Majaji wa ICC kumwachilia huru

Aliyekuwa kamanda wa kikosi cha waasi wa Uganda, LRA, Dominic Ongwen, akiwa katika mahakama ya ICC, 6 December 2016
Aliyekuwa kamanda wa kikosi cha waasi wa Uganda, LRA, Dominic Ongwen, akiwa katika mahakama ya ICC, 6 December 2016 ICC media outlet

Mawakili wa utetezi wa Dominic Ongwen, aliyekuwa kamanda wa kundi la wapiganaji la Lords Resistance Army (LRA), nchini Uganda, wamewaambia Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC, kumwachilia huru mteja wao.

Matangazo ya kibiashara

Katika utetezi wao, Mawakili hao wamesema Ongwen mwenye umri wa miaka 43, hakupenda kujiunga na kundi hilo kwa sababu alitekwa na kulazimishwa kujiunga na kundi la LRA akiwa mtoto na kuteswa sana.

Ongwen anakabiliwa na mashataka 70 yakiwa ni pamoja na mauaji na mateso, anayodaiwa kutekeleza akishirikiana na kiongozi wa LRA Joseph Kony, Kaskazini mwa Uganda miaka ya 2000.

“Domin Ongwen alikuwa mwathiriwa. Ukiwa mwathiriwa, utasalia kuwa mwathiriwa tu,” amesema Wakili wake Krispus Ayena Odongo.

“Watoto waliotekwa na LRA, walitumiwa katika vita Kaskazini mwa Uganda na wakawa katika mazingira magumu,” aliongeza.

Kiongozi wa LRA Joseph Kony ambaye amekuwa akitafutwa na kikosi cha kijeshi kutoka Marekani na Uganda lakini hajapatikana.

Inaaminiwa kuwa anaishi katika misitu nchini Sudan, DRC na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, watu 100,000 walipoteza maisha wakati kundi la LRA lilipokuwa likipambana na jeshi la Ugand ana kuwateka watoto zaidi ya 60,000 baada ya kuundwa miaka ya 1980.