UGANDA-SIASA-USALAMA-HAKI

Bobi Wine achukuliwa na polisi baada ya kurudi nchini Uganda

Mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayejulikana kwa jina la Bobi Wine kupitia muziki wa Pop, afanya mkutano na waandishi wa habari huko Washington, DC, Septemba 6, 2018.
Mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi, anayejulikana kwa jina la Bobi Wine kupitia muziki wa Pop, afanya mkutano na waandishi wa habari huko Washington, DC, Septemba 6, 2018. © AFP

Mwanamuziki maarufu wa zamani na Mbunge wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi anayefahamika kwa jina la Bobi Wine, amechukuliwa na polisi Alhamisi baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe akitokea Marekani ambako alikuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu, mke wake ameliambia shirika la habari la AFP .

Matangazo ya kibiashara

"Mara baada ya kuwasili katika mji wa Entebbe, vikosi vya usalama vilimzingira na kumpeleka," amesema Barbie Kyagulanyi. "Hatuna taarifa ya sehemu alikopelekwa," ameongeza.

Mapema nduguye Wine Eddy Yawe na naibu msemaji wa chama cha Democratic party Waiswa Alex Mufumbiro, walikamatwa na vikosi vya usalama na kuzuiwa kwenye kituo cha polisi uwanja wa Entebbe.

Msemaji wa polisi mjini Kamapala Luke Owoyesigyire, alionya kuwa yeyote ambaye atashiriki kwenye shughuli yoyote inayomhusu Bobi Wine atakamatwa

Robert Kyagulanyi aliondoka nchini Uganda tarhe 31 Agosti kwenda Marekani kwa ajili ya kupata matibabu baada ya kupigwa na kufanyiwa madhila mengine na maafisa wa polisi.

Tangu kuchaguliwa kwake katika Bunge mnamo mwaka 2017, Bw Kyagulanyi, mwenye umri wa miaka 36, ameibuka kama msemaji wa vijana wa Uganda na mkosoaji mkubwa wa Rais Yoweri Museveni, madarakani tangu mwaka 1986.

Bw Kyagulanyi alikamatwa na kufikishwa baadaye mbele ya mahakama ya kijeshi huko Gulu kwa kumiliki silaha kinyume na sheria, lakini mahakam ya kijeshi ilifuta mashitaka hayo. Hata hivyo alikamatwa tena kwa kosa la uhaini.