TANZANIA-KIVUKO-JOHN MAGUFULI

Miili ya watu tisa waliokufa kwa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere yazikwa Kisiwani Ukara

Eneo la Bwisya ambako miili tisa ya watu waliopoteza maisha kufuatia kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere imezikwa Septemba 23, 2018
Eneo la Bwisya ambako miili tisa ya watu waliopoteza maisha kufuatia kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere imezikwa Septemba 23, 2018 BBC

Miili ya watu tisa waliopoteza maisha kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere imezikwa hivi leo katika Kisiwa cha Ukara, Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Matangazo ya kibiashara

Maziko hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Aidha tukio hilo limehudhuriwa na baadhi ya wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya, maofisa wa serikali, vyama vya siasa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Miili hiyo tisa imezikwa kwa makubaliano baina ya serikali na familia za wahanga waliopoteza maisha huku serikali ikiahidi kujenga mnara wa kumbukumbu ya ajali hiyo mbaya kuikumba Tanzania katika miaka ya karibuni.

Miili mingine 172 ilitambuliwa na jamaa wa wahanga na kuchukuliwa kwa ajili ya maziko katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Katika hatua nyingine serikali ya Tanzania imeahidi kuunda tume ya uchunguzi kuhusu mkasa huo na kwamba wale  wote watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Aidha Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali ina mpango wa kuimarisha huduma ya usafiri katika visiwa mbalimbali vilivyomo katika wilaya ya Ukerewe.

Kivuko cha MV Nyerere kilichokuwa kikifanya safari zake kutoka Bugorola kwenda Ukara kilizama Septemba 20 kikiwa na zaidi ya watu 250 na kufikia leo juhudi za uokozi zimefanikiwa kuokoa watu 41 na kuopoa miili 224.