UGANDA-SIASA

Mugisha Muntu akihama chama chake cha siasa Uganda

Kiongozi wa zamani wa chama cha Forum Democratic Change (FDC) Jenerali Gregory Mugisha Muntu.
Kiongozi wa zamani wa chama cha Forum Democratic Change (FDC) Jenerali Gregory Mugisha Muntu. Mugisha Muntu/Twitter.com

Rais wa zamani wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda FDC, Jenerali Gregory Mugisha Muntu ametangaza kukihama chama hicho. Bw Muntu ametangaza kwamba ataandaa kikao na waandishi wa habari siku ya alhamisi.

Matangazo ya kibiashara

Muntu amesema amefikia uamuzi huo, baada ya mashauriano na wafuasi wa chama hicho na kushindwa kusuluhisha tofauti zake na rais wa sasa wa chama hicho Patrick Amuriat.

Mzozo ndani ya chama cha FDC ulifikia kilele chake na kufichuliwa hadharani mwezi Agusti, baada ya rais wa chama wa sasa Patrick Amuriat, kubadilisha uongozi wa chama cha FDC bungeni, na kuwafuta kazi waakilishi wake waliokuwa wameteuliwa na Mugisha Muntu, wakati alikuwa rais wa chama.

Mugisha Muntu, ambaye alikuwa rais wa chama hicho ametangaza uamuzi huo baada ya kikao na uongozi chini ya rais wa sasa Patrick Amuriat.

Ripoti zinasema kuwa, ameondoka ndani ya chama hicho na wabunge kadhaa waliochaguliwa kwa tiketi ya chama hicho lakini haijafahamika anahamia chama kipi.

Hata hivyo, Muntu hajatangaza mwelekeo wake mpya, lakini tayari kuna minong’ono kati ya raia wa Uganda kwamba anaelekea kushirikiana na mbunge Bobi Wine katika safari mpya ya kisiasa.

Muntu amekuwa mpinzani wa mara kwa mara wa Kizza Besigye wakati wa kumtafuta mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama hicho.