KENYA-AJALI-MAAFA-BASI

Kenya: Watu 50 wapoteza maisha katika ajali ya barabarani

Ajali ya barabarani katika barabara ya Kisumu kwenda Muhoroni Oktiba 10 2018
Ajali ya barabarani katika barabara ya Kisumu kwenda Muhoroni Oktiba 10 2018 www.standardmedia.co.ke

Watu 50 wamepoteza maisha na wengine 12 kujeruhiwa baada ya kutokea kwa ajali ya barabarani karibu na mji wa Kericho, Magharibi mwa Kenya. 

Matangazo ya kibiashara

Polisi wanasema basi la abiria linalofahamika kama Kakamega Homeboyz, lililokosa mwelekeo baada ya breki za basi hilo kukatika na kusababisha kubingiria mara kadhaa kwa basi hilo.

Kamanda wa Polisi katika eneo la Rift Valley, Zero Arome, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa waliojeruhiwa wamekimbizwa hospitalini.

“Abiria walikuwa wanasafiri kwenye Basi linaloitwa Kakamega Homeboyz, na waliojeruhiwa tumewakimbiza Hospitalini,” alisema Kamanda Arome.

Basi hilo lilikuwa limetoka jijini Nairobi kwenda mjini Kisumu na walioshuhudia wanasema, ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri siku ya Jumatano.

Jackosn Koskei mmoja wa mashuhuda ameliambia Gazeti la Daily Nation kuwa, alisikia sauti za abiria wakilia baada ya mlipuko mkubwa kusikika.

Miongoni mwa watu waliopoteza maisha ni watoto wanane, wote chini ya miaka mitano.

Ajali hii imetoa baada ya polisi wa trafiki kutoka ripoti inayoeleza kuwa ajali za barabarani zimeongezeka kwa asilimia nane mwaka huu nchini humo na zaidi ya watu 2,345 wamepoteza maisha.