TANZANIA-MOHAMMED DEWJI-USALAMA

Polisi nchini Tanzania yaendelea kumtafuta Mfanyabiashara mashuhuri, Mohammed Dewji, aliyetekwa Jijini Dar es Salaam

Mfanyabiashara mashuhuri nchini tanzania, Mohammed Dewji aliyetekwa Jijini Dar es Salaam
Mfanyabiashara mashuhuri nchini tanzania, Mohammed Dewji aliyetekwa Jijini Dar es Salaam forbes

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama nchini Tanzania vinaendelea na jitihada za kumtafuta Mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kwa jina la Mo aliyetekwa na watu wasiofahamika.

Matangazo ya kibiashara

Dewji ni tajiri kijana barani Afrika ambaye mbali na kumiliki kampuni mbalimbali chini ya kampuni mama ya Mohammed Entreprises Tanzanial Limited (MeTL), pia ni mwekezaji katika klabu maarufu nchini humo ya Simba, anamiliki asilimia 49 ya hisa.

Ripoti za mapema zimearifu kwamba Dewji 43 alitekwa katika hoteli moja Jijini dar es Salaam alikofika kwa ajili ya mazoezi alfajiri ya leo.

Tayari polisi ya Tanzania imeeleza kuwashikilia raia  wawili wa kigeni, ikiwatuhumu kuhusika na tukio hilo.

Vyanzo mbalimbali vya habari vimewanukuu mashuhuda wa kisa hicho wakisema watekaji walirusha risasi kadhaa hewani kabla ya kumchukua Dewji na kutokomea naye kusikojulikana.

Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika taarifa nyingine ameambia waandishi wa habari kuwa serikali itahakikisha Dewji anapatikana akiwa hai na salama na wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha uongozi wa klabu ya Simba umetoa taarifa ya kuwataka mashabiki wake kuwa watulivu na kujiepusha na ripoti zinachopishwa mitandaoni na badala yake watoe nafasi kwa vyombo vya dola kufanya kazi yake.

Aidha wachezaji wa klabu ya Simba kupitia kurasa zao  za mitandao ya kijamii wamekuwa wakitoa ujumbe wa kumtakia kheri Dewji, wakiomba arejee salama.

Aidha makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa Tanzania kwa ujumla wao wamemiminika mitandaoni wakilaani hatua ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo na kuvitaka vyombo vya usalama kuhakikisha anapatikana akiwa hai.

Mohammed Dewji ni nani hasa?

Ni mfanyabiashara mashuhuri nchini Tanzania na Februari mwaka huu alitajwa na Jarida la Forbes kuwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 1.4.

Amewahi kushika nafasi za kisiasa ikiwemo kuwa Mbunge wa jimbo la Singida Mjini kutoka mwaka 2005 hadi 2015.

Kwa mujibu wa tovuti yake mfanyabiashara huyo anajihusisha na biashara ya kuagiza na kusafirisha bidhaa ndani na nje ya Tanzania, biashara ya vyakula, mazao, vinywaji, usindikaji nafaka n.k

Baadhi ya mataifa ya Afrika ambako kampuni zake hufanya kazi ni pamoja na Burundi, DRC,Sudani Kusini, Rwanda, Zambia,Uganda, Ethiopia, Kenya.

Kampuni ya MeTL ni mojawapo ya kampuni binafsi zilizoajiri maelfu ya watanzania.