BURUNDI-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Mazungumzo baina ya Warundi: Serikali ya Burundi yaendelea kusubiriwa Arusha

Kikao cha tano na cha mwisho cha mazungumzo baina ya Warundi kinatarajiwa kufunguliwa Alhamisi wiki hii mjini Arusha nchini Tanzania. Hata hivyo serikali ya Burundi inaendelea kusubiriwa kushiriki mazungumzo hayo baada ya shughuli za ufunguzi wa mazungumzo hayo zilizokuwa zifanyike siku ya Jumatao kulazimika kusogezwa mbele.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akilindwa na askari wake wakati wa sherehe za uhuru wa Burundi.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akilindwa na askari wake wakati wa sherehe za uhuru wa Burundi. Onesphore Nibigira/AFP
Matangazo ya kibiashara

Licha ya ujumbe wa serikali ya Burundi kuchelewa kuwasili mjini Arusha, tayari wajumbe kutoka makundi mbalimbali ya upinzani yamewasili mjini Arusha.

Muungano wa vyama vya upinzani ulio uhamishoni CNARED umewasilishwa na kikosi kabambe kinachowajumuisha wanasiasa zaidi ya 5, ikiwa ni pamoja na Aliyekuwa kiongozi wa chama tawala CNDD-FDD na mbunge wa jumuiya ya Afrika Mashariki, Jeremie Ngendakumana, Leonard Nyangoma, Chauvineau Mugwengezo, Jeremie Minani, Pacrace Cimpaye...

Kwa upande wa muungano wa upinzani uliosalia nchini Amizero y'Abarudi, umewakilishwa na Agathon Rwansa, Pierre-Celestin Ndikumana.

Pia marais wa zamani wa Burundi Sylvetrse Ntibantunganya na Domitien Ndayizeye wamewasili mjini Arusha.

Serikali ya Burundi inasema haitaweza kushiriki katika mazungumzo hayo kwa kuwa nchi hiyo iko katika maombolezo ya mwezi mzima kuwakumbuka mashujaa wa taifa hilo kwa mujibu wa Evariste Ndayishimiye Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FD.

Kwa upande wao muungano wa upinzani wa ndani ya Burundi, Amizero y'Abarundi, unaoongozwa na Agathon Rwassa, ukieleza kushangazwa na hatua ya Serikali, ukisema utawala unatafuta sababu ili kukwepa mazungumzo ya Arusha.

Mazungumzo ya haya yanatajwa kuwa huenda yalikuwa ni ya mwisho katika kuelekea kupata muafaka kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kutoshiriki kwa Serikali ya Burundi,  kunaelezwa kuwa ni pigo kubwa kwa mratibu wa mazungumzo rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa.