BURUNDI-MAZUNGUMZO-SIASA-USALAMA

Benjamin Mkapa akosoa msimamo wa serikali ya Burundi

Benjamin Mkapa, Mratibu wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi.
Benjamin Mkapa, Mratibu wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi. EBRAHIM HAMID / AFP

Mratibu wa mazungumzo ya amani kuhusu Burundi, rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa, jana alifungua rasmi mazungumzo hayo huku akiikosoa Serikali ya Bujumbura kwa kukwamisha juhudi zake.

Matangazo ya kibiashara

Akiwahutubia wajumbe waliohudhuria, rais Mkapa amesema amesikitishwa na ombi lililotolewa na Serikali la kutaka mazungumzo haya yasogezwe mbele huku utawala ukijua fika kuhusu umuhimu wa mazungumzo ya safari hii.

Serikali ya Burundi yenyewe inasisitiza kuwa isingeweza kushiriki katika mazungumzo hayo kwa kuwa nchi inaomboleza na kwamba kile kinachojadiliwa sasa kitabaki kuwa makubaliano ya walioshiriki, na Serikali haihusiki.

Kwa upande wao upinzani unaona kuwa kutoshiriki kwa Serikali kumezidi kuwapa nguvu ya wao kuungana katika kuwa na kauli moja kuhusu hatma ya nchi yao.

Wajumbe wanaohudhuria mazungumzo yaliyong’oa nanga siku ya Alhamisi wanakutana faragha kwa makundi, na wamepewa siku 2 za kujadiliana kabla ya kurudi mezani kuwasilisha yale waliyokubaliana kwa mratibu wa mazungumzo.

Katika hatua nyingine umoja wa Ulaya umetoa taarifa kulaani kile kilichofanywa na Serikali ya Burundi, ambapo umetangaza vikwazo zaidi dhidi ya utawala wa Burundi.