BURUNDI-UN-SIASA-USALAMA

Michelle Bachelet aitaka Burundi kuheshimu Umoja wa Mataifa

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet. (Picha ya kumbukumbu).
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet. (Picha ya kumbukumbu). REUTERS/Lucas Jackson

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Michelle Bachelet ameitaka Burundi kuheshimu Umoja wa Mataifa na taasisi zake zote. Kauli hii inakuja siku moja baada ya balozi wa Burundi kufutilia mbali ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika nchi yake.

Matangazo ya kibiashara

"Taarifa ya jana ya Balozi wa Burundi Albert Shingiro dhidi ya ripoti ya Tume huru ya uchunguzi na ya Kimataifa iliyowekwa na Baraza la Haki za Binadamu inasikitisha sana," amesema Michelle Bachelet.

"Vitisho vya kuwafungulia mashitaka wajumbe wa Tume kwa kazi waliyofanya kwa ombi la Baraza la Haki za Binadamu- chombo kidogo cha Mkutano Mkuu - havikubaliki na vinapaswa kuondolewa mara moja," Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za Binadamu ameongeza.

"Kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Burundi inapaswa kuonyesha heshima kwa taasisi zake na idara zake mbalimbali, sheria na taratibu zilizowekwa na taasisi hiyo ya kimataifa," amesema Michelle Bachelet.

Siku ya Jumatano, akitoa madai yake mbele ya Tume ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, Albert Shingiro alifutilia mbali ripoti ambayo aliitaja kuwa "imepitwa na wakati, iliyotengenezwa kisiasa na lengo pekee ni kuhatarisha usalama wa nchi yake" akikanusha ushuhuda uliyotolewa akidai kwamba "hauna ukweli wowote".

"Hii ni ripoti iliyojaa uongo na yenye dharau". "Kutokana na uongo uliojaa kwenye ripoti hii, nchi yangu ina haki ya kuwafungulia mashitaka wahusika kwa kukashifu na kujaribu kuhatarisha usalama wa Burundi," Balozi wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa Albert Shingiro alisema.

"Zaidi ya miaka mitatu baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali na waasi na jaribio la mapinduzi lililotibuliwa na ambalo lilitengenezwa nje ya nchi mnamo mwaka 2015, Burundi inaendelea kudhulumiwa kisiasa na kidiplomasia," alisema Albert Shingiro.

Ripoti ya Tume Huru ya Uchunguzi iliyochapishwa mapema mwezi Septemba, inasema kuwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu, uliendelea nchini Burundi mwaka wa 2017 na 2018. Tume Huru ya Uchunguzi haijaruhusiwa kamwe kuingia nchi Burundi.

Mnamo mwezi Septemba Burundi ilisitishia kujitoa kwenye taasisi hiyo ikiwa "itaendelea kutumiwa kisiasa". Burundi mara kwa mara imekuwa ikiomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuondolewa kwenye ajenda ya vikao vyake, ikisema sio hatari kwa amani na usalama wa kimataifa.